Donald Trump Atangaza Majaribio Mapya ya Silaha za Nyuklia Marekani, Dunia Yapata Taharuki
Donald Trump ametangaza kwamba Marekani itaanza tena majaribio ya silaha za nyuklia, jambo lililoibua hofu na taharuki duniani. Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza mvutano kati ya Marekani, Urusi na China, na kuibua hatari ya vita vya nyuklia.
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba Marekani itaanza tena majaribio ya silaha za nyuklia, hatua inayoweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za usalama duniani. Kupitia ukurasa wake wa Truth Social, Trump aliandika: “Kutokana na mipango ya mataifa mengine kufanya majaribio ya silaha, nimeiagiza Wizara ya Ulinzi kuanza mara moja majaribio ya silaha zetu za nyuklia.” Trump alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla ya kukutana na Rais wa China siku ya Alhamisi, akisisitiza kuwa “mpango huo lazima uanze mara moja,” bila kufafanua ni wapi majaribio hayo yatafanyika.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine yenye silaha za nyuklia kama Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Korea Kaskazini, Marekani pia imekuwa na uwezo mkubwa wa kufanya majaribio ya teknolojia za nyuklia. Korea Kaskazini ndiyo nchi pekee iliyofanya majaribio ya nyuklia tangu miaka ya 1990, ingawa haijafanya hivyo tena tangu mwaka 2017. Ikulu ya White House haijatoa maelezo rasmi kuhusu tangazo la Trump, na bado haijajulikana ikiwa anamaanisha majaribio ya mifumo ya kurushia silaha hizo au majaribio ya silaha zenyewe.
Wataalamu wa masuala ya siasa na ulinzi wanasema hatua hiyo inaweza kuongeza hatari ya vita vya nyuklia duniani, hasa wakati ambapo mataifa makubwa yanaonekana kuingia katika ushindani mpya wa kijeshi. Jamie Kwong, mtaalamu kutoka shirika la Carnegie Endowment for International Peace, alisema: “Tuko katika kipindi cha hatari sana. Marekani, Urusi na China zinaweza kuingia kwenye mashindano mapya ya silaha za nyuklia.” Naye Darya Dolzikova kutoka taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI) nchini Uingereza, aliongeza kuwa kauli ya Trump “inaweza isiwe na athari kubwa kwenye mikataba ya sasa,” lakini ikazidisha mvutano wa kimataifa uliopo.
Kulingana na taasisi ya kimataifa ya utafiti wa amani SIPRI yenye makao yake Stockholm, Urusi ina silaha za nyuklia zipatazo 5,459, ikifuatiwa na Marekani yenye 5,177, na China ikiwa na takribani 600. Trump hata hivyo amedai kuwa Marekani “ndiyo yenye silaha nyingi zaidi duniani,” madai ambayo hayaendani na takwimu hizo.
Urusi hivi karibuni ilitangaza kuwa imefanya majaribio ya teknolojia mpya za kurushia silaha za nyuklia, ikiwa ni pamoja na silaha zinazoweza kusafiri chini ya maji hadi kwenye pwani za Marekani. Msemaji wa Kremlin alisema: “Ikiwa nchi yoyote itavunja mikataba ya kimataifa, Urusi nayo haitasita kufanya hivyo.” China, kwa upande wake, imesema inatarajia Marekani “kufuata makubaliano ya kimataifa ya kupiga marufuku majaribio ya silaha za nyuklia,” ikisisitiza kuwa Beijing “inazingatia msimamo wake wa kutojaribu silaha hizo.”
Daryl Kimball, mkurugenzi wa Arms Control Association mjini Washington, alionya kwamba kurejea kwa majaribio ya nyuklia kutakuwa kosa kubwa kihistoria. “Hatari ya vita vya nyuklia imeongezeka kwa miaka mingi. Bila mazungumzo kati ya Marekani, Urusi na China, dunia inaweza kuingia katika mashindano mapya ya silaha hatari zaidi,” alisema. Naye Hans Kristensen, kutoka Federation of American Scientists, aliongeza: “Binadamu wanapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa. Kwa mara ya kwanza tangu Vita Baridi, tunaona ongezeko la wazi la uzalishaji wa silaha za nyuklia.”
Marekani ilifanya jaribio lake la kwanza la bomu la nyuklia mnamo Julai 1945, katika jangwa la Alamogordo, jimbo la New Mexico. Baadaye ikawa nchi ya kwanza na ya pekee kutumia silaha za nyuklia katika vita, wakati mabomu yaliporushwa kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japani mwezi Agosti mwaka huo. Majaribio ya mwisho ya nyuklia ya Marekani yalifanyika mwaka 1992 katika mahandaki ya Nevada. Wataalamu wanasema itachukua angalau miaka mitatu kuandaa tena maeneo hayo kwa majaribio mapya. Kwa sasa, Marekani hutumia teknolojia za kompyuta za kisasa (simulations) kuchunguza ufanisi wa silaha zake bila kutumia milipuko halisi.
Rhys Crilley, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Glasgow, alisema: “Kama bado vita vipya vya nyuklia havijaanza, basi tuko karibu sana na mstari wake. Kila siku dunia inakaribia zaidi kwenye hatari ya vita vya nyuklia vya dunia.”


Kinyarwanda
English
Swahili



