Madagascar: Vijana Wameanzisha Tena Maandamano ya Kupinga Waziri Mkuu Mpya
Vijana wa nchini Madagascar wameamka na kuanzisha maandamano makubwa wakionyesha hasira na ghadhabu zao baada ya Rais mpya wa nchi hiyo, Kanali Michael Randrianirina, kutangaza tarehe 20 Oktoba kwamba amemteua mfanyabiashara Herintsalama Rajaonarivelo kuwa Waziri Mkuu mpya wa taifa hilo.
Herintsalama, Waziri Mkuu mpya wa Madagascar, hajapokelewa kwa furaha na wananchi wa taifa hilo, hasa vijana. Hata hivyo, amemrithi Ruphin Zafisambo, aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa zamani Andry Rajoelina, ambaye alipinduliwa madarakani wiki mbili zilizopita kufuatia vurugu kali zilizotikisa nchi hiyo.
Kanali Michael Randrianirina, rais mpya wa sasa nchini Madagascar, alipomteua Herintsalama Rajaonarivelo kuwa Waziri Mkuu tarehe 20 Oktoba 2025, alieleza kuwa alimchagua kutokana na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya uchumi na uhusiano wa karibu na mashirika mbalimbali ya kimataifa, akisema kuwa ataweza kusaidia katika kuinua uchumi wa taifa hilo.
Hata hivyo, maandamano mapya yaliyofanyika tarehe 21 Oktoba 2025, yakiongozwa zaidi na vijana waliokuwa mstari wa mbele katika maandamano yaliyomng’oa madarakani Rajoelina, yamepinga uteuzi huo. Waandamanaji hao walisema kuwa mabadiliko hayo ya Waziri Mkuu yaliyofanyika chini ya mwezi mmoja “hayana maana yoyote” na “ni kielelezo cha upendeleo na ukosefu wa haki,” kama walivyoiambia vyombo vikuu vya habari nchini humo.
Vijana hao wamedai kuwa Waziri Mkuu mpya ana uhusiano wa karibu na Kanali Randrianirina, rais wa sasa, jambo ambalo wanasema ndilo lililochangia kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo ya juu serikalini.
Hadi sasa, hali nchini Madagascar imezidi kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa utawala wa Rajoelina, kwani wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa haki za binadamu wanaendelea na maandamano makubwa wakipinga uteuzi wa Waziri Mkuu huyo mpya.
Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakiunga mkono maandamano hayo, wakisisitiza kuwa wanahitaji maelezo ya wazi kuhusu jinsi Rajaonarivelo alivyoteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Wananchi pamoja na viongozi hao wamesema wataendelea kuandamana hadi sauti ya wananchi itakapoheshimiwa na kusikilizwa.
Maandamano hayo nchini Madagascar yalianza mwezi Septemba, yakichochewa na matatizo ya kukatika kwa maji na umeme, lakini baadaye yakapanuka na kuwa harakati kubwa za kisiasa zilizochangia kupinduliwa kwa Rais Rajoelina aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu.
Kanali Randrianirina, ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Madagascar, aliingia madarakani wiki iliyopita baada ya kuapishwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoungwa mkono na maandamano makubwa ya wananchi waliokuwa wakimtaka Rajoelina ajiuzulu mara moja.
Kwa sasa, vijana wanaendelea na maandamano wakitaka serikali mpya ifanye mageuzi ya kweli yatakayowanufaisha wananchi wa Madagascar. Hata hivyo, Kanali Randrianirina amewaomba wananchi wawe na subira, akisema kuwa hatua zote anazochukua ni kwa manufaa ya taifa zima la Madagascar.
Vijana wa kizazi kipya Gen Z, ambao ndio waliopanga maandamano hayo, walifurahia sana baada ya utawala wa Rais Andry Rajoelina kupinduliwa.


Kinyarwanda
English
Swahili



