Nairobi: Kijana wa Miaka 19 Aliyepatikana Akiingia Bungeni Kinyume cha Sheria Adai ni Mwana wa Rais Ruto
Nelson Ibrahim Kidero, kijana wa miaka 19 aliyekamatwa katika majengo ya Bunge bila kibali, ameachiliwa na mahakama kwa masharti maalum. Kesi yake ilizua taharuki baada ya kudai kuwa yeye ni mwana wa Rais William Ruto.
Mwanamume mwenye umri wa miaka 19, Nelson Ibrahim Kidero, ameachiliwa huru na mahakama baada ya kupatikana akiwa katika majengo ya Bunge la Kenya bila kibali. Kijana huyo alizua mshangao mkubwa mahakamani kwa kudai kuwa yeye ni mwana wa kumzaa Rais William Samoei Ruto.
Kidero alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Benmark Ekhubi mnamo Alhamisi, Oktoba 9, akikabiliwa na shtaka la kuingia katika eneo la Bunge kinyume cha sheria — kosa linalokiuka Kifungu cha 31(1)(a) kwa kuambatana na Kifungu cha 31(2) cha Sheria ya Nguvu na Heshima za Bunge ya mwaka 2017.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kijana huyo alipatikana usiku wa Agosti 7, 2025, katika eneo la maegesho ya Bunge Towers bila ruhusa yoyote rasmi.
Kidero adai kuwa mwana wa Rais Ruto
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo mnamo Septemba 25, 2025, Kidero aliishtua mahakama kwa kauli yake ya kudai kuwa yeye ni mwana wa Rais Ruto.
“Mamangu anaitwa Angeline Muriithi. Bw. William Samoei Ruto ni babangu. Nilimsaidia kufikia nafasi yake ya sasa ya urais. Kwa hiyo, naamini kuna kosa fulani linaendelea bungeni,” Kidero aliambia mahakama kwa kujiamini.
Mahakama yatoa masharti magumu
Hakimu Ekhubi alimuachilia kijana huyo chini ya Kifungu cha 35(1) cha Kanuni ya Adhabu, lakini akasisitiza kuwa kuachiliwa huko kulikuwa na masharti makali.
“Hivyo basi, nitakuachilia chini ya masharti ya Kifungu cha 35(1) cha Kanuni ya Adhabu. Ukirudia kosa lolote, utahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela,” alisema Hakimu Ekhubi.
Kidero, ambaye pia anajulikana kama Nelson Muriithi, alikabidhiwa kwa mjomba wake Bw. Chege, na kuagizwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.
“Ninakukabidhi kwa mjomba wako, na masharti ni kwamba hutafanya kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja. Pia ni lazima uende kupokea matibabu,” aliongeza hakimu huku akimuuliza kijana huyo kama anakubaliana na masharti hayo.
Mahakama haikuzingatia madai ya uhusiano wake na Rais Ruto kwa kuwa hayakuwa sehemu ya mashtaka rasmi, lakini ilisisitiza umuhimu wa kijana huyo kupokea msaada wa kitabibu na uangalizi wa kifamilia.


Kinyarwanda
English
Swahili



